2 Juni 2026 - 20:24
Iran Yatoa Onyo Kali kwa Walowezi wa Kaskazini mwa Israel Endapo Beirut Itashambuliwa

Iran imeonya kuwa kushambuliwa kwa vitongoji vya kusini mwa Beirut kutakabiliwa na majibu makali, huku ikiwataka walowezi wa Kaskazini mwa Israel kuondoka katika maeneo hayo kwa ajili ya usalama wao iwapo mashambulizi hayo yatatekelezwa.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (AS) -ABNA-, Makao Makuu ya kijeshi ya Iran ya Khatam al-Anbiya yametoa onyo kali kwa walowezi wa Kaskazini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel, yakiwataka kuondoka mara moja iwapo utawala wa Israel utatekeleza vitisho vyake vya kushambulia vitongoji vya kusini mwa mji wa Beirut nchini Lebanon kwa madai ya kulenga harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hezbollah. 

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mashambulizi yoyote dhidi ya maeneo ya kusini mwa Beirut yatachukuliwa kuwa hatua ya hatari ya kuzidisha vita katika eneo hilo, na kwamba Muqawama pamoja na washirika wake hawatasita kujibu kwa hatua zinazofaa za kujilinda. Onyo hilo limekuja wakati mvutano kati ya Israel na Hezbollah ukiendelea kuongezeka kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel na vitisho vya kushambulia ngome za Hezbollah katika mji mkuu wa Lebanon.

Kwa mujibu wa duru za Iran, usalama wa wakazi wa Kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu unaweza kuwa hatarini endapo Israel itaendelea na sera ya kushambulia maeneo ya raia nchini Lebanon. Wakati huo huo, maelfu ya wananchi wa Lebanon wameendelea kuyakimbia maeneo ya kusini mwa Beirut kufuatia maonyo ya mashambulizi yaliyotolewa na jeshi la Israel.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha